Thursday 9 July 2015

KILIMO BORA CHA VITUNGUU MAJI-ONION PRODUCTION



KILIMO BORA CHA VITUNGUU MAJI

 

Vitunguu ni mojawapo ya zo muhimu ambalo hulimwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi Tanzania. Zao la vitunguu hulimwa kama zao la bishara katika maeneo mbalimbali nchini na huwapatia watu kipato kikubwa ambacho huwasadia katika kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kusaidia katika kupambana na umasikini. 
Vitunguu hutumika kama kiungo muhimu cha kuongeza harufu nzuri na ladha katika vyakula.  Hutumika katika utengenezaji wa supu, siki ,kachumbari nk. Majani ya vitunguu yana madini ya chokaa na wanga kwa wingi. Vilevile virutubisho vingine kama protini, chuma na ascorbic acidi hupatikana katika vitunguu.
Nchini mwetu vitunguu hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Tanga,  Arusha sehemu za Mang’ora na Babati, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Iringa wilaya ya Kilolo mpakani mwa mkoa wa Morogoro na kwenye maeneo ya mto Ruaha , Mara , Morogoro wilayani Kilosa sehemu za Lumuma na Malolo ,Mbeya Kilimanjaro na baadhi ya sehemu za Mkoa wa Singida.
Katika shamba lililo hudumiwa vizuri na kupandwa katika hali ya hewa na aina ya mbengu. Vitunguu hutoa kiasi cha tani (10) hadi 16 kwa ekari moja.
Mazingira
Vitunguu husitawi vizuri katika maeneo yenye miinuko kuanzia mita 800 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari. Hupendelea hali ya ubaridi kiasi hususani wakati wa kuotesha mbegu kati ya nyuzi joto 13 hadi 24°C ingawa kwa miche iliyoko kwenye kitalu joto zuri ni la nyuzi 20 hadi 27°C. Joto la juu hufanikisha utengenezaji wa kitunguu na ukaukaji. Hivyo ni vema vitunguu vioteshwe wakati wa baridi ili viweze kuvunwa wakati wa Joto.
Udongo: Huhitaji udongo tifutifu wenye rutuba nyingi usiotuamisha maji na usiopasukapasuka. Huhitai udongo ulio katika kipimo cha pH kati ya 6.0 na 7.0
Aina za vitunguu vinavyoshauriwa kuoteshwa katika ukanda wa Joto ni Red Creole, Texas Grano, Tropical Red F1 hybrid, Singida local na Pretoria Grano.

Baadhi ya aina ya vitunguu na sifa zake 


Aina
Siku za
kukomaa
Umbile la kitunguu
Rangi ya
ganda
Rangi ya
ndani
Red
Creole
150
Nusu bapa
Nyekundu
Nyekundu kahawia
Red
Bombay
160
Duara
Nyekundu angavu
Nyekundu kahawia
Texas
Grano
165
Duara
Njano (kaki)
Nyeupe




Upandaji na Uoteshaji miche
Mbegu za vitunguu huoteshwa kwanza kwenye kitalu kilichoandaliwa vizuri takribani wiki mbili. Vitunguu maji huoteshwa zaidi kwa kutumia mbegu kwenye kitalu na kisha kupandikizwa shambani.
Kabla ya kuzipanda mbegu. Tengeneza tuta lenye upana wa mita moja (sentimeta 100) na urefu wowote kutokana na mahitaji yako.  Weka mbolea aina ya samadi kiasi cha ndoo moja ukiichanganya vizuri na udongo kwa kila mita ya mraba moja.
Kiasi cha kilo 3.5 cha mbegu hutoa miche ya kutosha kupandikiza eneo la hekta moja ya shamba. Mwagilia kitalu kwa maji ya kutosha siku moja kabla ya kupanda mbegu.
Panda mbegu katika misitari yenye nafasi ya sentimita10 hadi 15 kutoka msitari hadi msitari Na kina cha sentimita moja kwa kumiminwa polepole kwenye mistari/mifereji iliyoandaliwa vizuri. Kisha fukia kwa kunyunyuzia udongo juu ya mbegu zilizoko kwenye mifereji.
Weka matandazo kisha mwagilia mara mbili kila siku(asubuhi na Jioni) hadi mbegu zitakapoota.Mbegu bora  huota baada ya siku 7 hadi 12 kutegema hali ya hewa. Mbegu huweza kuechelewa kuota hadi mpaka siku 21 udongo unapokuwa wa baridi sana na hali ya hewa ikiwa nzuri, mbegu huota mapema zaidi, hata ndani ya siku 4.

Kuandaa shamba
Tayarisha shamba vizuri mwezi mmoja kabla ya kupandikiza. Udongo utifuliwe vizuri kwenye urefu kina cha sentimita 30 na ulainishwe vizuri na majani yaondolewe kabisa. Mbolea za asili ziwekwe shambani ili kuufanya udongo ushikamane vizuri na uweze kuhifadhi mbegu. .Kisha tengeneza matuta au majaruba kufuatana na nafasi za kupandia ili kurahisisha umwagiliaji.
Kupandikiza vitunguu shambani
Miche huwa tayari kupandikizwa shambani wiki 6 hadi 9 kulingana na matunzo. Miche iliyo tayari huwa na urefu wa sentimita 12 hadi 15 na unene 1/2 au 3/4 ya kalamu ya risasi kwenye shina.
Kabla ya kupandikiza loanisha kitalu ili kuepuka kukata mizizi. Ng’oa miche kwa kutumia kijiti au chombo kingne na punguza majani na mizizi ili kusaidia kuzuia upotevu wa maji. Wakati wa upandikizaji chagua miche iliyo na afya nzuri ambayo haikushambuliwa na magonjwa na wadudu. Miche ipandwe wakati wa asubuhi na jioni ili kuepuka jua na joto kali linaloweza kuidhoofisha miche. Miche ipandikizwe kwenye nafasi ya upana wa sentimita 20 hadi 30 na nafasi ndani ya mstari ni sentimita 10 hadi 15. Baada ya kupandikiza mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka miche itakapo shika vizuri.


UTUNZAJI WA SHAMBA
A). Mbolea
Vitunguu vina hitaji udongo wenye rutuba ya kutosha ili viweze kusitawi vizuri.mbolea za kukuzia kama vile CAN au S/A ziwekwe shambani wiki 3 na ya 6 baada ya kupandikiza. Kiasi cha mifuko 3 au 4 kinatosha kuwekwa kwenye shamba la ukubwa wa hecta moja. Mbolea iwekwe katika kiwango sahihi yaani kifuniko kimoja cha soda (gram 5) kwa mche. Mbolea iwekwe kwenye mistari bila kugusa mche.
 
Upungufu wa kirutubisho cha Nitrojeni unaharakisha ukomaaji na unapunguza ukubwa wa kitunguu. Kirutubisho hiki kikizidi kupita kiasi huongeza ukubwa wa kitunguu na unene wa shingo ya kitunguu, tabia ambayo upunguza ubora.
B). Umwagiliaji:
Ili kupata mavuno bora shamba linatakiwa kuwa na maji ya kutosha kila wakati. Umwagiliaji wa maji yanayokwenda chini kiasi cha sentimeta moja (1cm) au zaidi kwa wiki ni mzuri kwa kupata vitunguu vikubwa. Epuka umwagiliaji kupita kiasi au pungufu kwani hali hii huweza kusababisha mipasuko. Punguza kumwagilia wakati vitunguu vinapokomaa kwani husababisha vitunguu vinavyokomaa kuoza.
C). PALIZI (UTHIBITI WA MAGUGU)
Magugu yaondolewe mara kwa mara kila yanapojitokeza hasa miche inapokuwa michanga.  Ukuaji na mavuno yanaathirika sana endapo magugu hayatadhibitiwa mapema. Magugu yanadhibitiwa kwa kutumia madawa ama jembe dogo la mkono. Wakati mwingine ni mchanganyiko wa madawa, jembe la mkono na kungolea kwa mkono.
MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
A). MAGONJWA
i.        Ubwiri vinyoya juu(powdery mildew) na wa chini (Downy mildew)
Huu husababishwa na ukungu na hupendelea hali ya unyevu nyevu. Hushambulia  hushambulia majani ya mimea iliyo shamabani na hata miche michanga. Dalili zake Kwenye majani kunaonekana vidoa vyeupe hasa kwenye majani makuu ya mimea michanga. Ukungu mweupe unatokea na kuongezeka kwa haraka kwenye sehemu au nyakati za baridi. Viini huishi kwenye mabaki ya mimea ya vitunguu na huweza kupeperushwa mbali na upepo.
Nyunyuzia dawa mojawapo zifuatazo kuzuia ukungu: - Dithane-M45, Ridomil, Topsin M70 na Cupric Hydroxide (Champion).
ii.      Ugonjwa wa doa la pinki (Purple blotch)
Huu nao ni ugonjwa uletwao na Ukungu na hushambulia majani, shingo na vitunguu vilivyokomaa. Huanza kama doa dogo linalozama ndani ya jani na kisha linaongezeka ukubwa na kufanya baka la rangi ya Zambarau ambalo huonekana katikati ya jani ambalo baadaye huwa jeusi. Shina lililoshambuliwa hulegea na kuanguka katika wiki ya tatu au ya nne baada ya dalili za ugonjwa kuonekana. Vitunguu vilivyokomaa huoza kuanzia shingoni na hugeuka rangi kuwa ya njano iliyochanganyika na nyekundu.

Zuia ugonjwa huu kwa kufanya yafuatayo:-
  •  Kupanda aina ya vitunguu visivyoshambuliwazidi na ugonjwa huu (Red Creole)
  •  Kubadilisha mazao
  • Vuna vitunguu kwa wakati sahihi
  • Matumizi ya mbolea zenye calcium, phosphate and potassium hupunguza kuenea kwa ugonjwa huu.
  •  Kwa upande mwingine,matumizi ya mbolea ya nitrojeni kwa wingi au kwa kiasi pungufu uongeza mlipuko wa magonjwa.
  • Viatilifu kama vile Mancozeb Dithane-M45, Ridomil, Topsin M70 na Cupric Hydroxide (Champion).

i.        Kuoza kwa shingo (Neckrot)
Husababishwa na ukungu na hupendelea vile vile hali ya unyevunyevu. Hushambulia zaidi vitunguu vilivyohifadhiwa. Ugonjwa huu husababisha vitunguu kuwa laini, hubonyea na huonekana kama vilivyopikwa. Huanzia kwenye shingo na baadaye huenea kwenye kitunguu chote na kufunikwa na ukungu wa kijivu.
Namna ya kuzuia:-
  • Vuna vitunguu kwa wakati sahihi  
  • Kubadilisha mazao 
  •   Tumia njia sahihi wakati wa kuvuna, epuka kuchubua au kukikwaruza wakati wa kuvuna
  •   Kausha vitunguu vizuri baada ya kuvuna
  •   Hifadhi vitunguu sehemu zisizo na unyevu mwingi

B). UDHIBITI WA WADUDU
Sata (Cutworms) Utitiri wa vitunguu (Onion thrips), Funza wa vitunguu (Onion maggots) na Minyoo wa vitunguu (Onion wireworms), Bungua weupe (White grub), ni miongoni mwa wadudu wasumbufu kwenye zao la kitunguu.
Tumia dawa zilizothibitishwa na wataalamu.
Uvunaji
Vitunguu huwa tayari kuvunwa baada ya miezi mitatu mpaka mitano (siku 90 mpaka 150) tangu kusia mbegu kutegemeana na aina na hali ya hewa ya eneo husika. Kabla ya kuvuna mkulima anaweza kuanza maandalizi ya kuvuna mwezi mmoja kabla kwa kuondoa udongo polepole kwenye kitunguu ili kusidia ukaushaji mzuri. Vitunguu vianze kuvunwa pale ambapo asilimia 50 hadi 75 ya vitunguu huonesha kulegea au kunyauka. Vitunguu huvunwa kwa hung’olewa na kurundikwa kwenye matuta na baadaye kukusanywa na kuwekwa kwa ajili ya kukata shingo. Mizizi pia inapunguzwa na vitunguu vinajazwa kwenye magunia tayari kwa kusafirishwa nyumbani kwa ukaushaji zaidi na kisha kuwekwa galani au kuuzwa.
 
KUHIFADHI
Vitunguu vilivyovunwa vikaushwe vizuri kabla ya kuvihifadhi. Vihifadhiwe katika eneo lenye hewa ya kutosha, isiyokuwa na unyevu wala jua kali. Vitutnguu vihifadhiwe kwa kuvitandaza juu ya chanja au kwa kufunga mashina yake yaliyokauka vizuri kwa kuyaning’iniza sehemu ya kuhifadhia. Vitunguu vinaweza kuhifadhiwa kwa miezi sita au zaidi bila kuharibika.
Mavuno
Mavuno ya vitunguu yanategeme huduma za shamba pamoja na hali ya hewa. Vitunguu pia hutofautiana katika mavuno kulingana na aina ya kitunguu. Kwa wastani vitunguu vinaweza kutoa mavuno kati ya tani 30 hadi 40 kwa hekta moja.

REJEAA
Dr MGEMBE. Onion Swahili brochure (Sokoine University of Agriculture (SUA))
The ministry of Agriculture, Food and Cooperative, extension department (2002)






 Kwa maoni au ushauri na maswali wasiliana nami kwa (SMS au kwa kwa kupiga) namba zifuatazo:-
                    
email: patsonjackson386@gmail.com